Acts 2

Kushuka Kwa Roho Mtakatifu

1 aSiku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja. 2 bGhafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3 cZikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. 4 dWote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.

5 eBasi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. 6Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. 7 fWakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? 8Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? 9 gWapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia, 10 hFrigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi, 11Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” 12Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”

13 iLakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!”

Petro Ahutubia Umati

14Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize. 15 jHakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! 16 kLa, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:

17 l“ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,
nitamimina Roho wangu
juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 mHata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu,
nao watatabiri.
19 nNami nitaonyesha maajabu juu mbinguni,
na ishara chini duniani:
damu, moto, na mawimbi ya moshi.
20 oJua litakuwa giza
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana
iliyo tukufu.
21 pNa kila mtu atakayeliitia
jina la Bwana, ataokolewa.’
22 q“Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 rHuyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani. 24 sLakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti. 25 tKwa maana Daudi asema kumhusu yeye:

“ ‘Nalimwona Bwana mbele yangu daima.
Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,
sitatikisika.
26Kwa hiyo moyo wangu unafurahia,
na ulimi wangu unashangilia;
mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini.
27 uKwa maana hutaniacha kaburini,
wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.
28 vUmenionyesha njia za uzima,
utanijaza na furaha mbele zako.’
29 w“Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa mpaka leo. 30 xLakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha enzi. 31 yDaudi, akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo,
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu.
32 aaMungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo. 33 abBasi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia. 34 acKwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,

“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
35 adhadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
36 ae“Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”

Waumini Waongezeka

37 afWatu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”

38 agPetro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 ahKwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”

40 aiPetro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 ajWale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.

Ushirika Wa Waumini

42 akNao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 alKila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 amWalioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 anWaliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 aoSiku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 apwakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.

Copyright information for SwhNEN